Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa
Amesema suala hilo la watumishi hewa limeisababishia serikali hasara kubwa hivyo ni lazima watu wote waliohusika katika mchakato huo wabainishwe na wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria za utumishi.
Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema hayo jana, alipokuwa akipokea taarifa ya maendeleo ya mkoa wa Lindi iliyowasilisha na mkuu wa mkoa huo, Godfrey Zambi katika siku ya kwanza ya ziara yake ya kikazi wilayani Ruangwa .
Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli wakati akiwaapisha wakuu wapya wa mikoa Machi 15 mwaka huu, aliwapa siku 15 kuhakikisha wanabaini watumishi hewa wote katika mikoa yao na kuwaondoa katika mfumo wa malipo.
Baada ya kufanyika kwa zoezi hilo jumla ya watumishi hewa 7,795 walibainika ambao wameisababishia serikali hasara ya sh. bilioni 7.5.
Waziri Mkuu amesema zoezi la kubaini watumishi hewa linalenga kuokoa fedha za serikali ambazo zilikuwa zinalipwa watumishi waliokufa, kustaafu wengine ni wale ambao wahusika walijiwekea majina na kisha fedha kuingia mifukoni mwa wajanja.
“Makatibu tawala wa mikoa ndio wakuu wa watumishi katika mikoa, hivyo ni lazima tusikie wamechukua hatua gani kwa wote waliosababisha kuwepo kwa watumishi hewa na si kukaa kungoja maagizo ya Rais,” alisema Mhe. Majaliwa.
Awali Mkuu wa mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi katika taarifa yake kwa Waziri Mkuu amesema mkoa huo una jumla ya wafanyakazi watoro 57 na hewa saba ambao ni marehemu, wastaafu waliokuwa wanalipwa mishahara na kuisababishia serikali hasara ya sh. milioni 36 kwa mwezi mmoja.
Amesema zoezi hilo la kubaini watumishi hewa na watoro litakuwa endelevu na wameanzisha timu kwa ajili ya kufanya uchunguzi ili kubaini sababu zilizosababisha watumishi waliokufa au kustaafu kuendelea kulipwa.