Monday , 28th Jan , 2019

Watuhumiwa 12 wakiwemo wafanyabishara wanne na Askari polisi nane waliohusika na utoroshaji wa madini aina ya dhahabu kilo 319.59 yenye thamani ya kiasi cha shillingi bilioni 27 kinyume na sheria ya usafirishaji wa Madini nchini leo wamefikishwa mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza.

Rais John Pombe Magufuli

Watuhumiwa hao wamefikishwa leo Mahakamani Jijini Mwanza ambapo kesi yao imekabidhiwa mbele ya Hakimu Mkazi Gwai Sumayi ambapo wanatuhumiwa makosa ya uhujumu uchumi, Rushwa pamoja na utakatishaji fedha.

Watuhumiwa hao wanatetewa na mawakili watano ambapo mtuhumiwa namba 2 na 3 wanatetewa na wakili wa kujitegemea Anthony Nasimir, huku wengine wanatetewa na Steve Makwega, wakili Fidelis Ntwewele, Nazario huku  upande wa serikali ukisimamiwa na Wakili Mwandamizi Castuce Ndamugoba.

Watuhumiwa wote 12 hawakutakiwa kujibu chochote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kusikiliza kesi hiyo na kurudishwa rumande hadi Februari 11 mwaka huu kesi itakapotajwa tena.

Akizungumza wakati akimuapisha Waziri wa Madini Dotto Biteko,  Rais Magufuli alifahamu njama zilizopagwa na baadhi ya askari polisi ambao walikuwa kwenye doria ambao walipanga kupokea bilioni moja ili kupitisha madini hayo.