Tuesday , 14th Feb , 2017

Mahakama ya Kazi nchini Kenya imewahukumu viongozi saba wa chama cha watumishi wa afya kifungo cha mwezi mmoja jela kwa kukaidi agizo la kumaliza mgomo ambao umedumu kwa zaidi ya miezi miwili.

Katibu Mkuu wa Chama Chama Madaktari Kenya Ouma Oluga (kushoto) akiwa na viongozi wenzake mahakamani kabla ya kuhukumiwa kifungo cha mwezi mmoja

Jaji Hellen Wasilwa amesema viongozi hao hawajatoa sababu za kutosha kuonesha ni kwa nini hawajamaliza mgomo huo ambapo pia ameamuru mazungumzo ya kumaliza mgomo huo yaendelee.

Awali Jaji Wasilwa aliwapa viongozi hao muda wa wiki mbili kumaliza mgomo huo, na baadaye akawaongezea siku tano na hata hivyo, mazungumzo ya kumaliza mgomo huo hata hivyo hayakuzaa matunda kipindi hicho.

Madaktari wamekuwa wakiitaka serikali kuheshimu makubaliano ya mwaka 2013 ya kuwaongezea mishahara.

Wamekataa mshahara walioongezewa na serikali wa asilimia 40 wakisema kuwa ni wa chini kuliko ule walioafikiana mwaka 2013.

Karibu madaktari na wauguzi 5000 kutoka hospitali 2000 za umma, walianza mgomo wiki ya kwanza ya mwezi Desemba mwaka jana.