Saturday , 25th Apr , 2015

Ofisa Afya wa Mkoa wa Njombe, Mathias Gambishi amewataka wakurungenzi wa halmashauri za miji ya Makambako na Njombe mji kurejesha fedha za kampeni ya afya na usafi wa mazingira zaidi ya milioni 42 walizozibadilishia matumizi yake.

Mkuu wa wilaya ya Njombe Sarah Dumba.

Gambishi alisema hayo wakati wa mkutano wa kiutendaji na utekelezaji wa kampeni ya usafi wa mazigira na afya, wa halmashauri ya wilaya ya Njombe mbele ya mkuu wa wilaya hiyo, Sarah Dumba na kumuomba kuwa amru wakurugenzi hao kuzirejesha fedha hizo ili zitumike kwenye mazingira.

Ameongeza kuwa Halmashauri ya Mji wa Njombe ilipewa shilingi milioni 31 na Makambako milioni 11 kwa ajili ya utekelezeji huo, na kwamba kama fedha hizo hazitarejeshwa wana mpango wa kuwaamrisha vijana wa Makambako na Njombe mjini kuandamana hadi kwenye ofisi za halmashauri hizo kudai fedha hizo.

Naye mkuu wa wilaya ya Njombe Sarah Dumba amesema atafuatilia jambo hilo na kuwa ni lazima halmashauri hizo zitekeleze kampeni hiyo.

Halmashauri ya wilaya Njombe ambayo iliongoza kwa usafi wa mazingira kitaifa mwaka jana kwa mara ya tatu, Dumba anawaagiza watendaji wa kata za Ninga, Mtwango na Ikondo kuongeza kasi ya utekelezeji wa kampeni.

Mkurugenzi wa halmashauri, Paul Malala na Afisa Afya wa Halmashauri hiyo, Remijius Sungu wameelezea mikakati ya kampeni hiyo.