Saturday , 8th Nov , 2014

Genge la wakulima na wafanyabiashara wapatao 66 wa wilayani Hanang na Babati mkoani Manyara limevamia ofisi ya Wakala wa Taifa Hifadhi ya Chakula (NFRA) wakiwashinikiza watendaji wa wakala huyo kuwalipa deni lao la mahindi

Genge la wakulima na wafanyabiashara wapatao 66 wa wilayani Hanang na Babati mkoani Manyara limevamia ofisi ya Wakala wa Taifa Hifadhi ya Chakula (NFRA) wakiwashinikiza watendaji wa wakala huyo kuwalipa deni lao la mahindi waliyoyauza kwake tangu mwezi Septemba mwaka huu, vinginevyo watachukua hatua za kumshtaki mahakamani kwa kuwa anawasababishia hasara kulingana na mikopo waliyoichukua.

Wakizungumzia deni lao baada ya kufika katika ofisi ya wakala huyo mjini Babati bila ya mafanikio aidha pia wakilazimika kufika ofisi ya mkuu wa wilaya hiyo kusikia kile ambacho mkuu wa wilaya hiyo Bw. Khalidi Mandia aliwaahidi kuwaeleza Pasipo mafanikio.

Wamedai kuchoshwa na ahadi za wakala huyo kwa kuwa tangu walipochukua mazao yao bila ya kuwepo kwa mkataba wa kukopeshana na kuwaacha njia panda,wameshindwa kulipa mikopo kwa wakati,aidha pia mbele yao wanashindwa kuandaa mashamba, huku wakidai hata Naibu Waziri wa kilimo Bw Godfrey Zambi aliwaahidi kulipwa kwa deni hilo mapema.

EATV imejaribu kufika katika ofisi ya wakala huyo, lakini hakuna afisa aliyeonekana kuwepo ofisini, huku Afisa Mtendaji wa wakala huyo Bw. Daniel Samuel muda mwingi akionekana kuongea na simu bila ya kutoa majibu, huku pia jitihada za kuwasiliana na meneja wa wakala taifa kanda ya Kaskazini Bw. Bright Mollel simu yake ikiwa haipatikani,hali ambayo pia licha ya wananchi hao kulalamikia Deni hilo,nao pia baadhi ya wafanyabiashara wa vyakula katika eneo hilo wameeleza kuathiri sehemu ya mitaji yao.

Katika ziara ya Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika Bw. Godfrey Zambi ya kutembelea vituo vya wakala wa taifa hifadhi ya chakula katika wilaya za Hanang na Babati Oktoba mwaka huu aliwataka wakulima na wafanyabiashara hao kuvuta subra na kuwahakikishia kuwa serikali italipa deni hilo la shilingi bilioni Saba mwishoni mwa mwezi Oktoba ama mapema mwezi wa Novemba mwaka huu kwani imeshapata takribani shilingi bilioni 30 toka benki ya CRDB na Wizara ya Fedha.