Kauli hiyo imetolewa leo na wakazi wa eneo hilo baada ya timu ya east Africa Radio kuwatembelea wakazi hao kujua hatua walizozichukua baada ya tamko la TMA, na kutoa msimamo wao juu ya suala hilo.
Akiongea kwa niaba ya wananchi wa eneo hilo Bi Aisha Kiloo amesema hawawezi kuhama eneo hilo kwani mafuriko hayo yanasababishwa na serikali kwa kutotatua chanzo kinacho sababisha mafuriko hayo, ambacho wamesema ni kufurika kwa mto msimbazi ambao unapita kwenye eneo hilo, hivyo kuitaka serikali ichimbe na kuongeza kina cha mto huo, ili kupunguza kasi ya kujaa kwa maji.
"Hapa sisi hatuhami, kwanza hatuna mafuriko, mafuriko yanasababishwa na mto msimbazi huu ukijaa, lakini serikali hawataki kuchimba, wachimbe waongeze kina cha urefu, hapo kidogo itasaidia, na sio kutuambia tuhame, hatuhami," alisema Bi Kiloo.
Pamoja na hayo wakazi hao wamelaumu wakandarasi wa kichina wanojenga bara bara maeneo hayo kwa kuziba mifereji inayopitisha maji kwenda baharini, hivyo kuongeza zaidi hali ya hatari pale mvua zinaponyesha.
Mamlaka ya hali ya hewa wiki hii imetoa taarifa ya kuwepo kwa mvua kubwa za elnino zinazotarajia kunyesha nchini, hivyo kuwataka wakazi wanaokaa maeneo ya mabondeni kuhama maeneo hayo, ili kunusuru maafa yatakayosababishwa na mvua hizo.
