Tuesday , 19th Jul , 2016

Adha ya uhaba wa maji safi na salama ni moja ya changamoto kubwa wanayokabiliana nayo wananchi wa kijiji cha Hiayari, halmashauri ya wilaya ya Mtwara hali ambayo inawalazimu kununua Ndoo moja kwa shilingi Miatano.

Mmoja wa wakazi wa Masasi Mtwara akichota Maji katika mto Nangoo kwa ajili ya matumizi ya Nyumbani

Wakizungumza na East Africa Radio kijijini hapo, wananchi hao wameiomba serikali kufanya jitihada za dhati kutatua tatizo hilo ambalo linawafanya washindwe kuoga na kufanya shughuli zingine zinazo hitaji huduma hiyo.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Mohamed Namkopa amesema kuwa tatizo hilo linatokana na uchakavu wa mitambo ya mradi wa Maji wa Mbuo-Mkunwa ambao awali ulikuwa unahudumia vijiji vichache kabla ya kufikia kutoa huduma kwenye vijiji 14, huku mwakilishi wa mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo Isack Bilali akidai wanaendelea na mikakati ya kutatua tatizo hilo.

Kijiji hicho kimezunguka kiwanda cha Saruji cha Dangote Industries Limited ambacho kuwapo kwake kimetoa matumaini makubwa kwa wananchi juu ya kupata ajira pamoja na kuondokana na kero mbalimbali za huduma za kijamii.

Sauti Mwenyekiti wa kijiji cha Hiyari, Mohamed Namkopa na mwakilishi wa mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Mtwara Isack Bilali.