Thursday , 24th Nov , 2016

Serikali imewataka wataalam wa tiba asilia ambao hawajasajiliwa kufuata taratibu za usajili ili waweze kutambulika na kupata usajili wa dawa zao kutokana na asilimia 60 ya watanzania kuhudumiwa kupitia tiba hizo.

Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya

 

Agizo hilo limetolewa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu, wakati akizindua fomu ya usajili wa dawa za asili ambapo ametaja taratibu za usajili kuwa ni pamoja na kusajiliwa kisheria na Baraza la Tiba Asili, kusajiliwa kwa kituo cha kutolea huduma pamoja na kuwasilisha taarifa zake katika ofisi ya Msajili wa Tiba Asili na Tiba Mbadala.

Amesema, mpaka sasa Baraza la Tiba Asili limefanikiwa kusajili waganga wa tiba asili zaidi ya 14,000 na vituo 180.

Amefafanua kwamba, pamoja na mafanikio hayo, baraza hilo kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za Serikali limeweka mfumo unaoweza kuwasaidia walaji kuhakikisha kuwa wanatumia dawa za asili zilizo salama kwa kuzipima katika maabara zinazotambulika na serikali.

Wakati huo huo Waziri Ummy amezindua kadi mpya za chanjo ya homa ya manjano baada ya kadi ya kwanza kuonekana ina baadhi ya mapungufu na kusema kuwa mpaka sasa Tanzania haijaripotiwa kuwapo kwa mgonjwa wa homa hiyo.