Tuesday , 24th Mar , 2015

Jumla ya wafungwa 54 Mkoani Dodoma wamenufaika na utaratibu wa kuwaachilia wafungwa ili wamalizie sehemu ya kifungo chao wakiwa katika familia zao (Parole) ambapo kati ya hao hakuna hata mmoja aliyerejeshwa gerezani kwa kuvunja masharti.

Mkuu wa mkoa wa Dodoma, Luteni Mstaafu Chiku Gallawa.

Hayo yamebainishwa leo na Mwenyekiti wa Bodi ya Parole Mkoa wa Dodoma, Balozi Job Lusinde wakati wa uzinduzi wa bodi mpya ya Parole Mkoa wa Dodoma.

Amesema jumla ya majalada 61 yalipendekezwa ambapo jumla ya wafungwa 54 walikubaliwa kuachiliwa kwa utaratibu wa Parole ambapo ni wafungwa wawili tu ndiyo waliokataliwa kutokana na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi alivyoona.

Balozi Lusinde amesema kuwa kati ya hayo majalada matano yalivyopendekezwa na bodi hiyo katika kikao chake cha Desemba 2014 bado wanasubiri uamuzi wa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi juu ya kuachiliwa kwao.

“Pia ninafurahi kukuarifu kuwa wafungwa wote 54 walionufaika na Parole hakuna hata mmoja aliyevunja masharti,” alisema Balozi Lusinde.

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Dodoma, Luteni Mstaafu Chiku Gallawa alisema kuwa azma ya serikali ya kuanzisha utaratibu wa parole ni kuwa mbinu mojawapo ya urekebishaji wa wahalifu yenye nguvu kwani ni sawa na kumweka mhalifu njia panda kati ya kuendelea na uhalifu au kujirekebisha na kumtaka achague mwenyewe ni njia ipi anayoamua kwenda.