Monday , 2nd May , 2016

Rais Magufuli amewataka wafanyakazi kuunga mkono juhudi za kuwafichua wanaozalisha wafanyakazi hewa, huku akibainisha kuwa mpaka kufikia jana jumla ya wafanyakazi hewa waliobainika walikuwa 10,293 ambao kwa mwezi mmoja tu wamelipwa sh bilioni 11

Rais wa Jamhuri wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli.

Akizungumza jana Mjini Dodoma katika sherehe za siku ya Wafanyakazi Dunia Rais Magufuli amesema kuwa kwa mwaka wafanyakazi hewa wamekuwa wakilipwa shilingi zaidi ya Sh. Bilioni 139, ambapo ukizidisha kwa miaka mitano wangelipwa zaidi shilingi bilioni 696.

Dkt. Magufuli ameongeza kuwa fedha hizo zinatosha kujenga madaraja kama la Nyerere lililopo Kigamboni, madaraja matatu, zinatosha kujenga flyover zinazojengwa Dar es salaam kwa msaada na mkopo kutoka Japan, huku akihoji endapo kama zingetumika kulipa mishahara ya wafanyakazi waliopo ndani ya serikali, tungewaongezea mshahara kiasi gani.

Dkt. Magufuli amesema kuwa kuna kipindi inafikia wakati suala la Wafanyakazi hewa ambao amewafananisha na "Shetani" wamfanye ajute kwanini aligombea nafasi ya urais lakini akawata watumishi na wafanyakazi wengine nchini wamsaidie katika kuwafichua watu hao ambao wanalitia taifa hasara ya mabilioni ya shilingi.

Aidha Rais Magufuli amezitaja taasisi zinaongoza kwa wafanyakazi hewa ni pamoja na Ofisi ya rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI),pamoja na serikali kuu

Hata hivyo Rais Magufuli amewahakikishia wafanyakazi wote ambao wanatekeleza majukumu yao kihalali kuwa serikali yake itawalinda na kuwatetea huku akitaka wawapuuze wanaodai serikali ya awamu ya tano haiwapendi wafanyakazi.

"Tukumbuke ya kuwa kazi ni utu, kazi sio fursa ya kupata mshahara kwa manufaa ya familia zetu bali ni fursa nzuri ya kutoa mchango kwa taifa lako kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho" amesema Dkt. Magufuli.