Wednesday , 23rd Mar , 2016

Wafanyabiashara ya mkaa Mkoa wa Morogoro wamelalamikia maafisa misitu wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro kwa kuwanyanyasa na kuwanyang’anya mkaa na pikipiki zao pamoja na kuwatoza faini hali inayosababisha waishi maisha magumu.

Mkaa ukiwa umepangwa tayari kwa kuuzwa

Malalamiko hayo yamekuja baada ya wakala wa huduma za misitu Tanzania (TFS), wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro kuendesha zoezi la kusaka na kukamata watu wanaouza na kusafirisha mazao ya misitu katika barabara ya Morogoro-Iringa pamoja na Morogoro -Dodoma na kufanikiwa kukamata magunia 161 ya mkaa pamoja na pikipiki 20 zilizokuwa zikitumika kusafirisha mkaa huo.

Wakieleza masikitiko yao baadhi ya wafanyabiashara wa mkaa wamelalamikia maafisa hao kuwanyanyasa kwa kuwanyang’anya mkaa kwani wanafanyabiashara hiyo kutokana na ugumu wa upatikanaji wa vibali vya kusafirisha na kuuza mkaa.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo meneja Misitu wa Wilaya ya Mvomero Bi, Husna Nzinyagwa, amesema Wilaya hiyo inakabiliwa na changamoto ya uvunaji mkaa na mbao hali inayopelekea uharibifu mkubwa wa mazingira na ameishauri serikali kuona uwezekano wa kupunguza bei za nishati ya mafuta na gesi ili wananchi wenye uwezo mdogo wa kiuchumi waweze kumudu na kutumia nishati hiyo kwa urahisi na mazingira yabaki salama.

Naye meneja msaidizi wa misitu wilaya ya Mvomero Bw. Sulemani Burenga amesema katika zoezi la doria hiyo wamefanikiwa kukamata idadi kubwa ya magunia ya mkaa na kwamba zoezi hilo ni endelevu na amewatahadharisha wale wote wanaofanya biashara ya mazao ya misitu bila kibali maalumu pamoja na waendesha pikipiki kuacha maramoja tabia ya kubeba mkaa kwani watakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo husika.