Friday , 15th May , 2015

Waandishi wa habari wa nchi za Afrika Mashariki wametakiwa kutumia vyema taaluma waliyonayo katika kulinda amani, kuandika habari kwa weledi na kusaidia katika kukuza demokrasia katika mataifa yao.

Wito huo umetolewa leo jijini Dar es salaam katika majumuisho ya semina ya siku mbili iliyowakutanisha waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali katika ukanda wa nchi za Afrika Mashariki yenye lengo la kujadili nafasi ya vyombo vya habari katika kukuza demokrasia.

Katika warsha hiyo miongoni mwa makubaliano yaliyoafikiwa na jopo la wawakilishi wa vyombo vya habari katika nchi ya Rwanda, Burundi, Kenya, Uganda na Tanzaniaa ni pamoja na kukuza sera ya umoja katika nchi za Afrika Mashariki, kuendeleza demokrasia pamoja na kutoa elimu ya kutosha kuhusu maandalizi ya uchaguzi katika nchi washirika.

Miongoni mwa hoja kubwa iliyojadiliwa katika Warsha hiyo ni pamoja na kutumika vibaya kwa vyombo vya habari na wanasiasa wakitolea mfano wa machafuko ambayo yanaendelea katika nchi ya Burundi ambapo wadau wa habari wamesema suala hilo lingeripotiwa vyema toka awali mgogoro uliopo baina ya pande za kisiasa usingekuwa mkubwa kama ulivyo kwa sasa.

Hata hivyo kwa upande wao wadau wa vyombo vya habari waliohudhuria mkutano huo wameeleza kuwa suala la kutowaendeleza na kutolipa kipaumbele suala la maadili na vyombo vya habari kuingiliwa na wanasiasa limesababisha udhoofishaji wa demokrasia huku wakidai vyombo vya habari kutokuwa na uwezo wa kifedha kutuma wawakilishi katika maendeleo yanayotajwa kuwepo na uvunjifu wa amani ili kutoa taarifa za kweli kuhusu vyanzo vya machafuko hayo.