Friday , 14th Aug , 2015

Bodi ya Mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu nchini Tanzania imesema kwa kipindi cha miaka 10 tangu ianzishwe imefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 74,

Naibu Mkurugenzi wa Elimu na Mawasiliano wa Bodi ya mkopo Bw. Cosmas Mwaisobwa

Bodi ya Mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu nchini Tanzania imesema kwa kipindi cha miaka 10 tangu ianzishwe imefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 74, licha ya changamoto kubwa ya kukosekana ushirikiano kwa baadhi ya waajiri katika kurejesha mikopo hiyo.

Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Naibu Mkurugenzi wa Elimu na Mawasiliano wa Bodi ya mkopo Bw. Cosmas Mwaisobwa ambapo ameongeza kuwa waajiri hawawajibiki katika kusaidia kuwatambua na kuwasilisha taarifa za wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu hivyo kuongeza idadi kubwa la deni la mkopo lisilolipwa.

Mwaisobwa ameongeza ni wajibu wa kila mnufaika wa mkopo wa elimu ya juu kurudisha mkopo anapomaliza masomo yake na kuwa bodi hiyo inatambua kuwa mwanafunzi yeyote aliyemaliza elimu ya juu anauwezo wakufanya kazi iwe ni rasmi au ya kujiajiri na kuwa kila mmoja anatakiwa akatwe asilimia nane ya mapato yake.

Akizungumzia changamoto nyingine wanazokumbana nazo katika utoaji wa mkopo na ukusanyaji wa madeni ni imani potofu ambayo imejengeka miongoni mwa wanufaika mikopo ni pamoja na kuwa na dhana kuwa fedha za mkopo ni ruzuku na kuwa wapo watu wenye uwezo wakujilipia wenyewe lakini kutokana na dhana ya kuwa ni ruzuku huomba ili wapate mikopo hiyo.

“Katika kutatua changamoto hii tumeweka mkakati wa utoaji elimu kuhusiana na fedha za hizo na kutumia mbinu za ziada zinazomlazimisha mnufaikaji kulipa mkopo wake kwa wakati” alisema.