Makamu wa Rais Dakta Mohamed Gharib Bilal.
Dakta Bilal ametoa changamoto hiyo Jijini Arusha katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela, ikiwa ni sehemu ya ufunguzi wa mkutano wa kimataifa wa vyuo vya elimu ya juu kutoka nchi kumi na nne za kiafrika ambao umeratibiwa na jumuiya ya vyuo vikuu vya nchini Sweden.
Akizungumza na wanazuoni chuoni hapo, dakta Bilal ambaye pia ni Mkuu wa Chuo cha Nelson Mandela kilichopo Tengeru nje kidogo ya Jiji la Arusha, amesema katika nyakati hizi ambazo kumeshuhudiwa mabadiliko makubwa yanayotokea ulimwenguni, ni vyema vyuo vya elimu ya juu katika nchi mbalimbali vikashirikiana katika utatuzi wa changamoto hizo.
Aidha Makamu wa Rais ameongeza kwamba licha ya Tanzania kupiga hatua kubwa katika Njanja ya elimu ya msingi kwa kuwafikia watu wengi zaidi, lakini kinachoangaliwa sasa ni kwa namna gani kutajengwa misingi imara katika nchi, ili kuzidi kukuza uelewa na ufahamu pamoja na matumizi ya sayansi na teknolojia kuhakikisha inachangia maendeleo kwa kasi kubwa zaidi.
Kwa upande wake waziri wa sayansi na teknolojia Profesa Makame Mbarawa amesema mambo yatakayojadiliwa katika mkutano huo, yanatarajiwa kuwasilishwa kwenye mkutano ujao unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao nchini Korea Kusini, huku baadhi ya wadau kutoa vyuo vya hapa nchini wakielezea mkutano huo kama hatua muhimu ya kuimarisha ustawi wa elimu inayotolewa Afrika.
Awali balozi wa Sweden nchini Lenarth Hjelmaker akizungumza katika mkutano huo amesema nchi yake imekuwa ikisaidia kuendesha tafiti na kukuza kiwango cha elimu ndani ya Afrika lengo likiwa ni kuhakikisha vyuo vikuu vinatumia fursa iliyopo kuwasaidia watu wa kawaida ndani ya Afrika.
Mkutano huo wa kimataifa unaojumuisha vyuo kumi na nne vya Sweden na nchi kumi na tano za Afrika, unafanyika katika chuo cha Nelson Mandela ambacho kimeanzishwa mahusussi kwaajili ya kanda ya Afrika mashariki kikiwa na hadhi ya kipekee katika Nyanja za elimu ya sayansi na teknolojia