Thursday , 8th Sep , 2016

Makamu wa Rais wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameiagiza Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kuhakikisha viongozi kuanzia ngazi za chini ikiwa ni pamoja na vijiji na kata wanajaza fomu za viapo vya uadilifu na kutangaza mali.

Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan (wa pili kushoto) akifungua ofisi ya sekretarieti ya maadili ya viongozi wa umma

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo leo mjini Mtwara wakati anafungua jengo la sekretarieti ya maadili ya viongozi wa umma Kanda ya Kusini ambalo ujenzi wake umegharimu takribani shilingi bilioni MBILI.

Makamu wa Rais amesema iwapo kama hatua hizo zitachukuliwa haraka zitakomesha na kupunguza kasi ya mmomonyoko wa maadili kwa viongozi na watumishi wa umma hali ambayo itaongeza uwajibikaji katika utendaji wa kazi miongoni watendaji hao.

Makamu wa Rais amewahimiza viongozi na watumishi wa umma kuthamini na wahakikishe walinda maslahi ya umma wakati wote wa utendaji wao wa kazi ili kuondoa malalamiko kwa wananchi.

Makamu wa Rais amesema ni jambo la muhimu kwa sekretarieti hiyo kufuatilia mienendo ya viongozi wa umma na kuwabaini wale wanaokwenda kinyume na misingi ya uadilifu na wachukuliwe hatua ipasavyo kabla hawaleta madhara kwa serikali na jamii kwa ujumla.

Makamu wa Rais pia ametoa rai maalum kwa wananchi wa mkoa wa Mtwara kuitumia ofisi hiyo mpya ya sekretarieti ya maadili ya viongozi wa umma Kanda ya Kusini kwa kutoa taarifa kuhusu mienendo ya viongozi wanaokiuka maadili ya umma katika utendaji wao wa kazi ili waweze kuchukuliwa hatua.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora Angela Kairuki amesisitiza kuwa kazi ya kuhakiki mali na madeni ya viongozi wa umma itaendelea kwa kasi nchini na mwaka huu sekretarieti hiyo itahakiki mali za viongozi wapatao 500 kote nchini.

Naye Jaji Mstaafu na Kamishna wa Maadili Nchini Salome Kaganda akitoa taarifa kuhusu ujenzi wa jengo hilo ameiomba serikali itenge fedha za kutosha kwa ajili ya kufanikisha zoezi la uhakiki wa mali na madeni ya viongozi kwa nchi nzima.

Makamu wa Rais pia ametembelea kiwanda cha kuchakata gesi cha Madimba, huku akitarajiwa kumaliza ziara yake hiyo wilayani Tandahimba hapo kesho.

Sauti ya Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan
Sauti Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora Angela Kairuki