Sunday , 7th Feb , 2016

Wakati shirika la kuhudumia watoto duniani, UNICEF likisema kuwa watoto na wanawake wapatao milioni 200 katika nchi 30 wamekumbwa na ukeketaji, FGM nchini Tanzania harakati za kutokomeza mila hiyo potofu zimeanza kuzaa matunda.

Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF), Koshuma Mtengeti.

Koshuma Mtengeti ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Children Dignity Forum nchini humo linaloendesha shughuli zake kwa ushirikiano na shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu, UNFPA ametaja mafanikio hayo kuwa ni pamoja kuanzisha vilabu vya wasichana..

Hata hivyo amesema changamoto ni pamoja makazi ya kudumu kwa wasichana waliokimbia mila ya ukeketaji akisema makazi ya sasa ni ya muda.

Katika taarifa yao ya siku ya kupinga ukeketaji, wakurugenzi wa UNFPA na UNICEF wanasema ukeketaji unachochea ubaguzi dhidi ya wasichana na wanawake na mwezi Septemba kwenye mkutano wa maendeleo endelevu mataifa 193 yaliafikiana malengo mapya ya kutokomeza ukeketaji ifikapo 2030, hali ambayo imethibitisha kwamba ukeketaji ni janga la kimataifa.