Wednesday , 1st Jun , 2016

Mkoa wa Mtwara umefanikiwa kuwakusanya vijana 156 waathirika wa madawa ya kulevya na kati ya hao, vijana 104 tayari wameunganishwa katika mpango wa matibabu katika hospitali ya rufaa mkoani humo, Ligula.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Halima Dendego akipokea Mwenge wa Uhuru.

Hayo yameelezwa mkoani humo na Mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego, baada ya kukabidhiwa Mwenge wa Uhuru na mkuu wa mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi, katika Tarafa ya Mpapura, halmashauri ya wilaya ya Mtwara, kabla ya kumkabidhi mkuu wa wilaya ya Mtwara, Fatma Ally.

Aidha, amesema ukiwa mkoani Mtwara, Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kuzindua jumla ya miradi 40 katika halmashauri zote tisa na wilaya tano za mkoani humo yenye thamani ya Sh. Bilioni 49.8 huku mchango wa wananchi ukiwa ni Sh. Bilioni 1.8 katika fedha hizo.

Awali akizungumza kabla ya kukabidhi Mwenge huo kwa mkuu wa mkoa wa Mtwara, mkuu wa mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi, alisema Mwenge huo ukiwa mkoani mwake uliweza kuzindua jumla ya miradi 48 yenye thamani ya Sh. Bilioni 11.6.

Kwa upande wake, mkuu wa wilaya ya Mtwara, Fatma Ally akizungumza baada ya kukabidhiwa Mwenge huo na mkuu wa mkoa wa Mtwara, amesema katika wilaya yake Mwenge utakimbizwa kwa siku mbili huku miradi 12 yenye thamani ya Sh. Milioni 12 ikitarajiwa kuzinduliwa.

Sauti ya Mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego akizungumzia tatizo la madawa ya Kulevya