Monday , 1st Aug , 2016

Ukubwa wa mtaji katika Soko la Hisa la Dar es Salaam DSE umeongezeka kwa asilimia mbili kutoka fedha za Tanzania shilingi trilioni 23.5 hadi shilingi trilioni 24 kwa mujibu wa taarifa ya mauzo katika soko hilo kwa kipindi cha juma moja lililopita.

Meneja Miradi na Biashara wa DSE Bw. Patrick Mususa

Meneja Miradi na Biashara wa Soko hilo Bw. Patrick Mususa amesema katika kipindi hicho, ukubwa wa mtaji wa makampuni ya ndani nao pia umeongezeka kwa asilimia 1.8 kutoka shilingi trilioni 8.2 hadi shilingi trilioni 8.3.

Mususa amesema hata mauzo sokoni hapo yameongezeka kwa zaidi ya mara tano hadi kufikia shilingi bilioni 21.6 kutoka shilingi bilioni nne kwa juma huku idadi ya hisa zilizouzwa na kununuliwa pia ikiwa imepanda kwa asilimia 43 khadi Milioni 3.9 kutoka Milioni 2.7.

Kwa upande wa viashiria, kumekuwa na ongezeko la pointi mbili kwenye sekta ya viwanda baada ya bei za hisa za TCCL kupanda kwa asilimia 5.88 ingawa bei za hisa za TOL na TPCC zilishuka kwa asilimia 0.62 na 0.87 rasmi.

Sekta ya huduma za kibenki na kifedha hii imepanda kwa pointi 191 baada ya bei kupanda kwenye kaunta za NMB (14.88%) na DSE (7.48%) huku sekta ya huduma za kibiashara ikiwa imebakia kwenye kiwango kile kile cha kama ilivyokuwa juma lililopita.