Thursday , 31st Jul , 2014

Umoja wa Katiba ya Wananchi UKAWA umeendelea na msimamo wake wa kutorejea katika vikao vya bunge maalumu la Katiba ikiwa zimebaki siku chache kabla ya kuanza kwa vikao vya bunge hilo.

Baadhi ya viongozi wa wabunge wa bunge maalumu la Katiba kutoka kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi UKAWA.

Viongozi wa UKAWA wametoa msimamo huo jijini Dar es Salaam leo licha ya viongozi mbalimbali wa dini nchini kutoa wito kwa wajumbe wa UKAWA kulegeza msimamo wao na kurejea katika Bunge maalum la Katiba.

Wakizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, viongozi wa UKAWA wamesema wanawaheshimu viongozi wa dini lakini wameshangazwa jinsi viongozi hao wa dini wanavyoshindwa kuzungumzia lugha za kejeli, matusi, pamoja na kibaguzi unaofanywa na baadhi ya wabunge wa bunge hilo hasa wale wa kutoka chama tawala CCM.

Mmoja wa wenyeviti wa UKAWA Prof. Ibrahim Lipumba amesema ili warejee bungeni kujadili rasimu ya Katiba ni lazima maoni ya wananchi yaheshimiwe pamoja na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi CCM waliotoa kauli za ubaguzi,kejeli na matusi wachukuliwe hatua.

Naye Mwenyekiti Mwenza wa UKAWA Mhe Freeman Mbowe amesema kwa sasa hawapo tayari kurejea katika bunge hilo huku akishangazwa na kauli zinazotolewa na viongozi mbalimbali wa CCM licha ya kuwa katika mazungumzo ya kutafuta suluhu ili kurejea katika Bunge maalum la Katiba kwa maslahi ya Taifa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti Mwenza wa UKAWA, Mhe. James Mbatia amasema endapo mchakato wa Katiba mpya utakwama yafanyike marekebisho machache ya msingi katika Katiba ya sasa ikiwa ni pamoja na kuundwa kwa tume huru ya uchaguzi