Saturday , 2nd Aug , 2014

Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) umeendelea kushikilia msimamo wake wa kutorejea katika Bunge La Katiba, baada ya mazungumzo yaliyokuwa yakifanyika baina ya umoja huo na Chama Cha Mapinduzi CCM kuvunjika.

Viongozi wakuu wa UKAWA

Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) umeendelea kushikilia msimamo wake wa kutorejea katika Bunge La Katiba, baada ya mazungumzo yaliyokuwa yakifanyika baina ya umoja huo na Chama Cha Mapinduzi CCM kuvunjika.

Katika taarifa iliyotolewa leo na viongozi wakuu wa umoja huo na kusomwa kwa waandishi wa habari na mwenyekiti mwenza Freeman Mbowe, mazumzo hayo yaliyolenga kusuluhisha mgogoro uliopo kati wajumbe wa UKAWA na wale wa CCM, yalivunjika jana usiku yakiwa katika hatua zake za mwisho.

Mazungumzo hayo yaliyokuwa chini ya msajili wa vyama vya siasa nchini Jaji Francis Mutungi, yalianza Julai 3, mwaka huu, na yalikuwa katika awamu nne kabla ya kuvunjika rasmi katika awamu ya Nne.

Viongozi hao wamesema sababu kubwa ya mazungumzo hayo kuvinjika ni CCM kutokuwa na nia ya dhati ya kutafuta suluhu.
“Hatua yetu hii inafuatia mfululizo wa matukio yaliyoonesha wazi kwamba, zaidi ya kututaka turudi kwenye Bunge Maalum bila masharti yoyote, CCM haikuwa na nia ya dhati katika mazungumzo hayo” inasomeka sehemu ya taarifa yao.

Wamesema katika vikao vitatu viongozi wa CCM wakiongozwa na katibu mkuu wa Chama hicho walihoji mara kwa mara mamlaka ya msajili wa vyama vya siasa kuitisha na kuratibu mazungumzo hayo na kuibua vikwazo mara kwa mara.

Sababu nyingine ya kuvunjika kwa mazungumzo hayo, wamesema kuwa ni kuanzishwa kwa mazungumzo mapya chini ya mwenyekiti wa Bunge Maalum Samwel Sitta ambayo hayakuwa katika utaratibu maalum, na wameshangazwa na kitendo cha Rais kikwete kumpongeza Samwel Sitta kwa hatua hiyo.

Wakizungumzia hotuba ya Rais Kikwete, wamesema kuwa, Rais Kikwete amepotosha ukweli kuhusu sababu zilizowafanya UKAWA kususia Bunge Maalum.

Wamesema kuwa, katika hotuba yake, Rais Kikwete vilevile amepotosha matumizi ya kanuni ya 33(8)(i) cha kanuni za Bunge Maalum kuhusu mamlaka ya Bunge hilo, na kukwepa kuzungumzia mabadiliko ya Kanuni yaliyofanywa na bunge April 25, baada ya UKAWA kutoka.

Katika taarifa hiyo, UKAWA Wameendelea kusisitiza kuwa wanachokitaka ni kuona Bunge Maalum linatekeleza majukumu yake kisheria ambayo ni kujadili, kuboresha na kupitisha Rasimu ya katiba ya jamhuri ya muungano wa Tanzania, iliyoandaliwa na Tume ya mabadiliko ya katiba, kutokana na maoni ya wananchi na sio kuibomoa, kuibatilisha na kuifuta Rasimu hiyo na kuweka Rasimu wanayodai kuwa ni ya CCM.

Wamesema kuwa, CCM wameendeleza msimamo ulioelezwa na Rais Kikwete katika hotuba yake kwamba mamlaka ya Bunge Maalum hayana mipaka.

Mwisho wamesema: “UKAWA hatuko tayari kuendelea na mazungumzo na CCM wala kurudi katika mkutano wa Bunge Maalum kwa kuwa kufanya hivyo ni kusaliti maoni ya wananchi na kutumia vibaya fedha za umma kubariki uchakachuaji wa msingi (Essentials Features) wa Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume,”

Kuhusu ni hatua gani watachukua baada ya kuvunjika kwa mazungumzo hayo, taarifa yao inasema “Katika hatua ya sasa tunaanza mazungumzo miongoni mwa viongozi wa wajumbe wa UKAWA na katika wakati muafaka tutaueleza umma maamuzi mbadala tutakayoyafanya kwa kuwezesha kupatikana kwa katiba ya wananchi”