Magdalena Sakaya - Naibu Katibu Mkuu CUF
Chama cha Wananchi (CUF), kimesema hakikushiriki kikao cha jana cha UKAWA kutokana na sababu za kikatiba za ndani za chama hicho kwa sababu wao kama chama bado wanajadiliana ili kuafikiana kwa maslahi mapana ya taifa kama vyama vingine vinavyofanya na sio kweli kwamba wamejitoa katika umoja huo.
Akizungumza leo Jijini Dar es Salaam Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Bara Mhe. Magdalena Sakaya amesema kwa sasa wamekuwa na vikao vinavyojadili kwa upana juu ya namna watakavyogawana madaraka endapo wakishinda uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba.
Akizungumzia nafasi ya mgombea urais anayependekezwa na chama hicho ,Mhe. Sakaya amesema Mwenyekiti wa chama CUF Prof.Ibrahim Lipumba aliposema wamtangaze mgombea urais wa UKAWA Julai 14 mwaka huu alikiuka vikao vya maamuzi vya chama hicho ambavyo vilikuwa bado havijakaa kutoa maamuzi.
Aidha akiwa katika kipindi cha HOT MIX cha EATV, Magdalena Sakaya amesema kuwa UKAWA bado haijapata mgombea urais na kuongeza kuwa chama hicho hakitambui taarifa iliyotolewa na baadhi ya viongozi wa UKAWA kuhusu kupatikana kwa mgombea ambaye anasubiri utambulisho rasmi.
Sakaya amesema kwa mujibu wa taratibu za UKAWA, wagombea wote wanapaswa kwanza kupitishwa na vyama vyao, halafu wakutane pamoja kama UKAWA kuamua ni yupi agombee, jambo ambalo halijafanyika hadi sasa.
"Katika mkutano wa jana sisi CUF hatukuwepo, sasa wanasema wamempata mgombea urais, watampataje bila chama kimoja kuwepo? ukweli ni kwamba bado mgombea wa UKAWA hajapatikana, lakini atapatikana baada ya taratibu tulizojiwekea kufuatwa" Amesema Sakaya.