Friday , 29th Jan , 2016

Wilaya ya Longido ni kati ya wilaya kame nchini zinazokabiliwa na uhaba wa mvua pamoja na upungufu wa maeneo ya malisho ya mifugo hali inayosababisha migogoro kati ya wakulima na wafugaji .

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido,Felix Kimariyo

Wananchi wa Longido wametakiwa kutumia taarifa za mabadilko ya hewa kwa kutenga maeneo ya malisho kulingana na msimu wa mvua na kuepusha migongano isiyo ya lazima.

Hayo yameelezwa na mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Longido, Felix Kimariyo wakati wa mafunzo ya jinsi ya kutumia taarifa za mabadiliko ya hali ya hewa kwa wakulima,wafugaji na wataalamu wa sekta mbalimbali ili kuchochea maendeleo ya jamii.

Mchumi Mwandamizi wa wilaya ya Longido Ally Msangi na Mfugaji Nangole Mbiriki wamesema kuwa zaidi ya asilimia 90% ya wakazi wa Longido hutegemea shughuli za ufugaji kama njia kuu ya kuwaongezea kipato hivyo amewataka wafugaji na Halmashauri kutumia taarifa za mabadilko ya hali ya hewa katika kupanga mipango ya uchumi na kukabiliana na changamoto za mabadiliko hayo.

Mkurugenzi wa utafiti na matumizi ya hali ya hewa Dkt Ladislaus Chang`a amesema kuwa wananchi hawana budi kujenga tabia ya kuvuna maji ya mvua, kupanda miti kama njia ya kurejesha uoto wa asili ambao baada ya kutoweka umesababisha mabadiliko ya tabia ya nchi.

Wilaya ya Longido inakabiliwa na changamoto ya uharibifu wa mazingira ikiwemo ukataji miti, uchomaji mkaa pamoja uchafuzi wa mazingira mambo yanayosababisha mabadiliko ya tabia ya nchi na ongezeko la joto duniani, hivyo kila mwananchi ana jukumu la kuyalinda mazingira na kuyanusuru na uharibifu wa aina yoyote ile.