Waziri wa Maliasili na Utalii nchini Tanzania, mh. Lazaro Nyalandu.
Fedha hizo zitatolewa kupitia taasisi inayojishughulisha na uhifadhi wa wanyama na rasilimali za misitu ya Frankfurt Zoological Society (FZS) na kwamba msaada huo utakuwa tayari mapema mwakani.
Mratibu wa Frankfurt Zoological Society nchini Tanzania Bw. Gerald Bigurube ameiambia EATV kuwa makubaliano juu ya utolewaji wa fedha hizo yameshasainiwa na kwamba fedha hizo zitatumika kujenga uwezo wa kukabiliana na ujangili katika hifadhi ya wanyamapori ya Selous na mbuga ya Serengeti.
Mapema mwaka huu, taasisi hiyo ya FZS ilitoa magari kumi aina ya Land Rover 110, kwa serikali ya Tanzania, magari yaliyogharimu zaidi ya shilingi milioni 250 za Tanzania.
Aidha katika hatua nyingine, juhudi za kukabiliana na wimbi la uwindaji haramu wa wanyama jamii ya Tembo zinaonesha kuzaa matunda nchini Tanzania ambapo katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita hakujawahi kutokea kwa tukio lolote la kuuawa kwa wanyama jamii ya Tembo.
Waziri wa Maliasili na Utalii Mh. Lazaro Nyalandu amesema hayo katika mahojiano na EATV moja ya sababu za mafanikio hayo kuwa ni kutokana na juhudi za pamoja kati ya serikali na wahisani za kukabiliana na vitendo vya ujangili.
Juhudi hizo kwa mujibu wa waziri Nyalandu ni pamoja na Operesheni Tokomeza pamoja na miradi kadhaa inayotekelezwa kwa kushirikiana na wahisani ambayo kwa pamoja imelenga kukabiliana na ujangili pamoja na ulinzi wa maliasili za misitu.
Kwa mujibu wa Waziri Nyalandu, idadi ya wanyama jamii ya Tembo nchini imeendelea kupungua kwa kasi kwani takwimu zilizochukuliwa mwaka 2012 zinaonyesha idadi yao imepungua na kufikia Tembo 13,000 kutoka Tembo 70,000 waliokuwepo miaka kumi iliyopita.