Tuesday , 6th Oct , 2015

Tafiti zinaonesha kuwa nyumba zote zilizojengwa bila kukamilika hapa nchini thamani yake ni kubwa kuliko fedha zote zilizopo kwenye mabenki kwa kuwa watumishi wengi hupoteza fedha zao katika ujenzi usiokamilika na kuchukua muda mrefu.

Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Makazi kwa watumishi wa Umma Dkt. Fredrik Msemwa

Hayo yamesemwa na afisa mtendaji mkuu wa kampuni ya makazi kwa watumishi wa umma Dkt. Fredrik Msemwa wakati akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam na kuongeza kuwa kujenga nyumba kwa fedha binafsi ni ghali kuliko kukopa mkopo wa nyumba wenye gharama nafuu.

Dkt. Msemwa amesema kuwa watumishi wengi wa umma huishia kuishi maisha magumu kwa sababu fedha zao nyingi hupotea katika ujenzi usiokamilika na unaochukua muda mrefu.

Dr Msemwa ameongeza kuwa kuna uhitaji wa nyumba bora zaidi ya million moja na laki mbili hapa nchini huku mkoa wa Dar es salaam pekee zikihitajika nyumba zaidi ya laki nne.

Aidha Dr. Msemwa amesema kuwa kampuni hiyo ya makazi kwa ajili ya watumishi wa umma itasaidia watendaji wa serikalini na watu binafsi kuishi katika nyumba bora kwa gharama nafuu..