Sunday , 6th Apr , 2014

Wakazi wa jimbo la Chalinze mkoa wa Pwani nchini Tanzania, leo wanapiga kura kumchagua mbunge wa jimbo hilo katika uchaguzi mdogo unaofanyika kuziba nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo marehemu Saidi Bwanamdogo.

Kinyang'anyiro kikubwa katika uchaguzi wa leo ni kati ya vyama hasimu vya Chadema na CCM ambapo Chadema kinawakilishwa na Bw. Mathayo Tondorey huku Ridhiwani Kikwete akigombea kupitia chama tawala yaani CCM.

Msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo Bw. Samwel Malyanga amesema hali ya uchaguzi huo ni shwari na vituo vyote 288 vimefunguliwa ambapo amewataka wakazi wa jimbo hilo ambao wana sifa za kupiga kura wajitokeze kushiriki zoezi hilo la kidemokrasia.

Kuwepo kwa utulivu na amani kumethibitishwa pia na katibu msaidizi wa idara ya uenezi wa CCM Bw. Suleiman mwenda, ambaye amesema mpaka sasa hawajaona tukio lolote linaloashiria uvunjifu wa amani.