Friday , 21st Aug , 2015

Makamu wa Rais Dkt. Mohammed Gharib Bilali ameihakikishia dunia kuwa serikali ya Tanzania ina dhamira ya dhati ya kumaliza tatizo la usafirishwaji haramu wa binadamu.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilali .

Dkt. Bilal ameyasema hayo leo mbele ya Mabalozi na wawakilishi wa mashirika mbalimbali yanayopinga usafirishwaji haramu wa binadamu waliohudhuria uzinduzi wa sheria ya kuzuia usafirishaji haramu wa binadamu na Mpango kazi wa kitaifa wa mwaka 2015-17 wa kumaliza tatizo hilo.

Dkt. Bilal ameongeza kuwa kuwa tatizo hilo ni kubwa duniani kote ambapo takwimu zinaonesha kuwa watu laki saba husafirishwa kiharamu toka nchi moja kwenda nchi nyingine kwa ajili ya kutumikishwa kazi za mashambani, majumbani na hata kazi za ngono na ugaidi haswa vijana, watoto na wasichana.

Kwa upande wake waziri wa mambo ya ndani Mathiasi Chikawe amesema kuwa tafiti zinaonesha kuwa Tanzania inatumika katika upitishaji wa wahamiaji haramu kwenda nchi nyingine za Afrika, Ulaya na Mashariki ya mbali.