Tuesday , 10th May , 2016

Serikali imesema kuwa itahakikisha inatengeneza mfumo mzuri katika sekta ya afya katika ngazi za chini ili kusaidia sekta za juu ziweze kutoa huduma zinazohitajika na kuokoa maisha ya wananchi hususani ya wakina mama na watoto.

Naibu Waziri wa TAMISEMI, Mhe. Suleiman Jaffo.

Akizungumza leo Bungeni Mjini Dodoma katika kipindi cha maswali na majibu Naibu Waziri wa TAMISEMI, Mhe. Suleiman Jaffo, amesema kuwa lengo la kufanya hivyo ni kuzipunguzia mzigo wa wagonjwa hospitali za rufaa ili ziweze kutoa huduma kwa ubora unaotakiwa.

Mhe. Jaffo amefafanua hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Segerea,Mhe Bona Kalua, ambae alihoji changamoto ya huduma za afya katika maeneo yake ikiwemo ukosefu wa vituo vya afya kwa sehemu kubwa.

Naibu Waziri huyo amesema serikali inalifanyia kazi suala ambalo lipo katika mpango wa Wizara ya Afya na kuongeza kuwa kuna baadhi ya matibabu yanaweza kupatikana katika vituo hivyo endapo vitaboreshwa katika utoaji huduma.

Mhe. Jaffo amesema kuwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili inaonekana kuzidiwa na wagonjwa kutokana na kutokuwa na mifumo mizuri kwa ngazi za chini katika sekta ya afya jambo ambalo serikali haina budi kuanzia chini kufanya marekebisho hayo.

Sauti ya Naibu waziri wa TAMISEMI, Mhe Suleiman Jaffo akiongelea Uboreshaji sekta ya Afya