Tundu lissu
Akiongea leo Juni 28, 2019 bungeni, wakati wa kuhitimisha mkutano wa kumi na tano, kikao cha hamsini na tano kilichoambatana na hoja ya kuahirisha bunge, Spika amesema, amemjulisha Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kujaza nafasi hiyo.
''Napenda kuwafahamisha waheshimiwa wabunge kuwa kiti cha ubunge cha jimbo la Singida Mashariki kilichokuwa kinashikiliwa na Mh. Tundu Lissu kipo wazi na nimemjulisha Mwewnyekiti wa Tume ya Uchaguzi aendelee na taratibu za kukijaza'', amesema.
Ndugai amefafanua kuwa kutokana na Tundu Lissu, kushindwa kutoa taarifa kwa spika kwa muda wote ambao hayupo bungeni, pamoja na kutowasilisha tamko la mali zake anakuwa amevunja sheria ya uchaguzi.
''Kifungu cha 37, kifungu kidogo cha 3 cha sheria ya taifa ya uchaguzi sura ya 343, kinanitaka kumtaarifu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi nini cha kufanya''.
Aidha spika ameongeza kuwa ni zaidi ya mwaka mmoja umepita, ambapo Tundu Lissu amekuwa akionekana kwenye vyombo mbalimbali vya habari katika nchi tofauti, huku akiwa hajafika bungeni wala kutoa taarifa yoyote kwa spika au kupitia kwa uongozi wake kitu ambacho ni kinyume na Katiba.
Spika wa Bunge, Mhe. Job Ndugai amemwandikia barua Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kumtaarifu kuwa Jimbo la Singida Mashariki lipo wazi kufuatia aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo Mhe. Lissu kutokuwepo bungeni bila taarifa, na pia kutojaza fomu ya tamko ya mali na madeni.
— Bunge la Tanzania (@bunge_tz) June 28, 2019