Wednesday , 4th Nov , 2015

Jeshi la polisi limesema kuwa limejipanga kikamilifu kulinda usalama wa raia na mali zao katika tukio la kuapishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli hapo kesho.

Kamishna wa Oparesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi Paul Chagonja

Akiongea na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa makao makuu ya jeshi la polisi nchini, Paul Changonja amewataka wananchi kutoa taarifa pindi wanapoona dalili za uvunjifu wa amani.

Mbali na hilo Kamishna Chagonja alivishukuru vyombo vya habari kwa kutoa ushirikiano na kuhabarisha umma kwa weledi na kuimarisha amani ya nchi na kuvitaka kuendelea kufanya hivyo wakati wote.

Katika hatua nyingine jeshi hilo limepiga marufuku maandamano ya aina yoyote nchini yanayopangwa kufanywa na vikundi vya siasa kwa lengo la kushinikisha kutangazwa kwa wagombea wao kupitia viti vya ubunge na madiwani ikiwa ni pamoja na kushinikiza tume ya uchaguzi Zanzibar ZEC kutangaza mshindi.

CP Paul Chagonja ameongeza kuwa tayari jeshi la polisi limewakamata watuhumiwa wa maandamano hayo yaliyofanyika baadhi ya maeneo nchini bila kupata vibali halali vya polisi.

Chagonja amesema kuwa ni wajibu wa wananchi wote kuendelea kuheshimu sheria za nchi na kujiepusha na vitendo vya aina yoyote ile ambavyo vinaweza huhatarisha usalama wa raia na mali ikiwemo maandamano yanayopangwa kufanyika bila kufuata utaratibu.