Thursday , 25th Dec , 2014

Tume ya Rais ya Uchunguzi wa Operesheni Tokomeza itakusanya taarifa na kupokea malalamiko yaliyotokana na utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili nchini mikoa ya Mikoa ya Arusha, Manyara, Tabora, Singida na Dodoma.

Katibu wa Tume ya Operesheni Tokomeza, Bw. Frederick Manyanda.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa tarehe 24 Desemba, 2014 na Katibu wa Tume hiyo, Bw. Frederick Manyanda, Tume inatarajiwa kuendelea na zoezi la kukusanya maoni na taarifa kuanzia tarehe 5 Januari , 2015 mpaka tarehe 21 Januari,2015 katika maeneo mbalimbali ya kanda ya Kaskazini na Kati Nchini.

Katika kutekeleza jukumu hilo, Bw. Manyanda ameeleza kuwa, Tume itatembelea Mkoa wa Tabora tarehe 4 Januari 2015 mpaka tarehe 8 Januari 2015 na itakuwa Mkoa wa Singida tarehe 9 Januari,2015 mpaka tarehe 10 Januari,2015.

Aidha Tume itatembelea Mkoa wa Dodoma tarehe 11 Januari, 2015 mpaka tarehe 12 Januari 2015. Vilevile, Wakili Manyanda ameeleza kuwa Tume itakusanya maoni Mkoa wa Manyara kuanzia tarehe 13 Januari, 2015 mpaka tarehe 16 Januari, 2015 na Tume itakuwa Mkoa wa Arusha tarehe 16 Januari 2015 mpaka tarehe 19 Januari,2015.

Mpaka sasa Tume ya Rais ya Operesheni Tokomeza imefanikiwa kukusanya taarifa na kupokea malamiko yaliyotokana na utekelezaji wa Operesheni Tokomeza katika mikoa kumi na tano (15) ya Tanzania Bara ambayo ni Kigoma, Katavi, Rukwa, Mbeya Kagera, Geita, Shinyanga, Simiyu, Mwanza, Mara, Lindi, Mtwara, Ruvuma, Iringa, Morogoro.

Pamoja na mikutano hiyo, Bw. Manyanda ametumia fursa hiyo kuwakumbusha na kuwaomba wananchi na watanzania wa maeneo husika kuendelea kutuma taarifa na malalamiko kuhusu utekelezaji wa Operesheni Tokomeza kwa njia ya barua, simu na barua pepe ambapo ameeleza kuwa wananchi wanaweza kutuma barua kwa Katibu wa Tume, Tume ya Uchunguzi wa Operesheni Tokomeza Ujangili.