Katibu Mkuu wa UNCTAD, Dkt. Mukhisa Kituyi
Dkt. Kituyi amesema hayo Mjini Nairobi nchini Kenya, kabla ya mkutano huo unaotarajiwa kufunguliwa na mwenyeji Rais Uhuru Kenyatta na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon ambapo amewafananisha wawekezaji hao wapya kama wacheza kamari.
Hivyo ametoa pendekezo ili kuepusha zahma kama iliyotokea nchini Argentina ambako wawekezaji wa aina hiyo huondoa fedha zao bila kujali umma na kwenda kuwekeza kwenye faida zaidi.
Mkutano wa 14 wa hufanyika kila baada ya miaka minne ambapo lengo ni kukipatia chombo hicho mamlaka mpya na hutanguliwa na majukwaa mbalimbali ikiwemo lile la bidhaa.
Katika jukwaa la bidhaa lililohitimishwa Jumamosi, ripoti ya UNCTAD imebainisha kuwa nchi zinazotegemea kuuza nje bidhaa ili kujipatia fedha za kigeni hupoteza asilimia 67 ya mapato ya mabilioni ya dola ya biashara hiyo kutokana na ankara za biashara zinazoandikwa kidanganyifu.
Ripoti hiyo inatokana na utafiti wa miongo miwili kutoka Chile, Cote d’Ivoire, Nigeria, Afrika Kusini na Zambia ikiangazia bidhaa kama vile kakao, dhahabu, mafuta na shaba kutoka nchi hizo.
Dkt. Kituyi akizungumzia ripoti hiyo amesema inadhihirisha jinsi udanganyifu kwenye ankara za biashara unavyochochea usafirishaji haramu wa fedha na kuathiri maendeleo ya nchi hizo zinazotegemea kipato kutokana na kuuza nje bidhaa zake.
Ripoti hiyo inaonesha mwelekeo wa nyaraka zisizo sahihi kwa mauzo ya bidhaa za nje kuelekea nchi kama vile China, Ujerumani, Hong Kong(China), Italia, India, Japan, Uholanzi, Hispania na Marekani.