Dkt Kikwete ameyasema hayo katika sherehe za maadhimisho ya miaka 38 ya chama hicho zilizofanyika katika uwanja wa Majimaji mjini Songea, ambapo amesema kuwa Katiba Inayopendekezwa ni miongoni mwa Katiba bora duniani.
Dkt Kikwete amesema Katiba hiyo imezingatia maslahi mapana ya Taifa na kugusa makundi yote katika jamii, wakiwemo wakulima, wafugaji, wavuvi, vijana, wanawake na kila mtanzania maslahi yake yamezingatiwa.
“Kwa maoni yangu sioni sababu ya kuikataa Katiba hii, ina kila kitu….. Ni bora kuliko Katiba ya sasa…. Tukiikataa tutarudi kwenye Katiba ya sasa……., tutakuwa tumeikataa na mazuri yake yote…. Nawasihi watanzania wote tuiunge mkono” amesema Kikwete.
Katika hatua nyingine Dkt Kikwete ameeleza kusikitishwa kwake na kauli ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi UKAWA ya kutangaza kususia upigaji kura ya maoni kwa ajili ya kupitisha Katiba Mpya.
Amesema “Kauli hiyo imenisikitisha sana ingawa haikunishangaza kwa kuwa hata wakati wa Bunge la Katiba walifanya hivyo”
Amesema “Jambo la busara wanalotakiwa kufanya UKAWA ni kuwashawishi watu kupiga kura ya HAPANA lakini mimi naamini kuwa kura za NDIYO zitakuwa nyingi”
Amewaagiza viongozi wa CCM kote nchini kutambua kuwa wana jukumu la kuwaelimisha watanzania wote kuipigia Kura ya Ndiyo Katiba hiyo, kwa kuwa UKAWA watakuwa wanatoa Elimu hasi ya kuwashawishi watanzania kuikataa Katiba.
Dkt Kikwete amesema kuwa hoja pekee waliyonayo UKAWA ni idadi ya serikali, “Hoja yao ni serikali tatu, hawana hoja zaidi ya hiyo, eti kwa kuwa serikali tatu haimo basi wanasema Katiba haifai… hawana hoja zaidi ya hiyo, watanzania tusiwasikilize….”
Kuhusu muda uliobaki, Dkt Kikwete amesema kuwa tume ya Uchaguzi inasimamia kila kitu na wametoa uhakika kuwa kufikia katikati ya mwezi April watakuwa wamekamilisha zoezi la kuandikisha wapiga kura kwa mfumo wa BVR.
“Jambo la msingi viongozi wote wa CCM wahamasisheni watu kujitokeza kujiandikisha kwa kuwa usipojiandikisha kwa mfumo huu mpya hautapiga kura ya maoni wala kura katika uchaguzi mkuu.
Ameongeza kuwa ni muhimu Katiba Mpya ikapatikana wakati wa uongozi wake kwa sababu hatujui kama Rais ajaye atakuwa na hamu ya kuwa na Katiba mpya kama ilivyokuwa yeye.
“Mimi nilipata hamu ya kupata Katiba mpya, huwezi jua Rais ajaye kama atakuwa na hamu kama mimi…. Yeye anaweza kusema kipaumbele chake ni kujenga nchi na siyo Katiba….. Kwahiyo ni muimu kuipata sasa…”