Tuesday , 10th Nov , 2015

Mtandao wa Jinsia nchini Tanzania(TGNP) umesema kuwa unategemea serikali iliyoingia madarakani itatekeleza ahadi zake pamoja na kuzingatia usawa wa kijinsia katika kuundwa kwa Serikali kutokana na Tanzania kusaini Mikataba mbalimbali ya kimataifa.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Bi. Lilian Liundi.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Lilian Liundi amesema watanzania wengi wanategemea utekelezwaji wa ahadi za viongozi walizozitoa wakati wanaomba kura na kukamilika kwa ahadi hizo kwa mujibu wa mikataba mbalimbali ya kikanda na kimataifa.

Aidha Mkurugenzi huo amebainisha kuwa wanatarajia serikali mpya chini ya Rais Dkt. John Magufuli itatekeleza kwa vitendo ahadi hizo hususani katika kuwateua wanawake zaidi katika nafasi za juu za uongozi kwenye mihimili mikuu mitatu ya serikali ambayo ni Mahakama, Baraza la mawaziri na Bunge.

Katika hatua nyingine watetezi hao wamewataka wanawake wote waliochaguliwa kwenye nafasi za uongozi ubunge na udiwani kuwajibika kikamilifu katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuwatendea haki wananchi kwa usawa.