
Mbwana Samatta ambaye aliwasili katika uwanja wa Julius Nyerere majira ya saa nane usiku alilakiwa na viongozi wa serikali, Viongozi wa TFF, familia yake ikiongozwa na baba yake na mama yake pamoja na mamia ya wananchi.
Baada ya mapokezi hayo ya kifani shirikisho la mpira wa miguu nchini liliongoza msafara hadi katika hoteli ya Serena iliyopo posta jijini Dar es salaam ambapo Sammatta amelipiwa kupumzika katika hoteli hiyo kwa muda wa siku mbili.
Wakiwa hotelini hapo mkurugenzi wa idara ya michezo Bi Juliana Yassoda aliiwakilisha serikali kwa kumpongeza Samatta kwa kuwatoa watanzania kimasomaso katika mashindano hayo yaliyovuta hisia za watu wengi duniani.
Hata hivyo TFF imesema imeandaa dua maalumu Alhamisi Januari 14 ya kumuombea Samatta katika uwanja Karume, dua ambayo itahudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini na wa serikali pamoja na wananchi.
Aidha TFF imewataka watanzania na wadau mbalimbali wanaotaka kumpongeza Samatta kufanya hivyo lakini TFF ipewe taarifa kuhusiana na jambo hilo.