Sunday , 13th Dec , 2015

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania(TCRA), imekusudia kuwafutia leseni wamiliki wa Radio na Televisheni wanaokwepa kulipa ada zao sambamba na kwa makampuni ya simu yanayoshindwa kutoa huduma bora za mawasiliano kwa watanzania.

Mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya mawasiliano nchini, Dkt. Ally Yahaya Simba

Mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya mawasiliano nchini, Dkt. Ally Yahaya Simba amewataka wamiliki wa vyombo vya habari kuhakikisha wanalipa ada zao za leseni na madeni mengine wanayodaiwa kabla ya Dec. 30 mwaka huu,vinginevyo wataanza kufungiwa.

Aidha Dkt. Simba amewataka wamiliki wa mitandao ya simu za mkononi wanao toa huduma zao chini ya kiwango na ubora unaotakiwa kutoa huduma nzuri kwani kwenda kinyume watakabiliwa na adhabu kali sambamba na kuwafikisha mahakamani wote watakao toa huduma mbovu.

Nao wadau wa mawasiliano mkoani morogoro wamewasilisha malalamiko mbalimbali kwa mamlaka hiyo hasa kwa upande wa mitandao ya simu za mkononi kukatà ovyo mawasiliano au kukata fedha tofauti na matumizi pamoja na kushindwa kushughulikiwa matatizo yao kwa muda muafaka.

Wengine wamehoji matumizi ya watangazaji wasio na taaluma na weledi wakiwemo wanaoanzisha vipindi vilivyo kinyume na maadili ya mtanzania sambamba na usumbufu wa kutumia ving'amuzi vingi tofauti katika matumizi ya TV