Akitoa taarifa hiyo Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Joseph Masikitiko amesema, vipimo vya maabara vya sampuli ya mafuta hayo vimeonesha kuwa hayafai kwa matumizi.
Alisema hayo ni matokeo ya ukaguzi wa hivi karibuni wa shehena hiyo yenye ujazo wa tani za metriki 38,521.018 katika meli ya MT. Ridgebury John B, yaliyokuwa yasambazwe na kuuzwa nchini.
Alisema, "Vipimo vinaonesha kuwa baadhi ya matakwa ya viwango vya mafuta ya petroli hayajafikiwa, hivyo kuamuru yarejeshwe yalikotoka. Kiwango cha ubora cha mafuta ya petroli ni TZS 672:2012/ EAS 158:2012 ambacho hakikufikiwa".
Matakwa ya kiwango ambacho mafuta hayo hayakukidhi ni pamoja na kuwa na kemikali zilizo na oksijeni ndani yake ambazo husababisha madhara kwenye injini za magari na mitambo.
Alifafanua kuwa mafuta hayo yameonekana kuwa na uwezo mkubwa wa kuvuta maji au mvuke na kuwa sehemu ya petroli, kiasi cha kuifanya iwe na maji mengi ambayo ni hatari kwa injini za magari na mitambo.
Aliwahakikishia watumiaji wa mafuta kuwa, shirika hilo litahakikisha linafanya ukaguzi katika meli zote zenye mafuta yanayokusudiwa kusambazwa nchini ili kuzuia yasiyo na ubora yasiingizwe sokoni.