Monday , 3rd Sep , 2018

Hivi karibuni Mkuu wa Wilaya Kisarawe, Jokate Mwegelo, amekuwa akionekana kushupalia suala la elimu wilayani humo, lakini sasa amehamia kwenye idara ya maji ambapo amesema tatizo la maji kwa wanakisarawe lipo mbioni kubaki historia.

Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo akiwa ofisini kwake.

Jokate ameweka wazi kuwa wamewekeza nguvu zaidi katika kusimamia ujenzi wa mradi wa maji kutoka Kibamba hadi Kisarawe kwa kushirikiana na DAWASA. Ameeleza kuwa Mei 2, 2018 serikali kupitia DAWASA ilisaini mkataba na mkandarasi kutoka China Henan International Cooperation Group (CHICO), wenye thamani ya Tshs 10.05 billioni kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo.

Mkataba huo unajumuisha ujenzi wa toleo pamoja na kituo cha kusukuma maji (boosting station), ambapo zitafungwa pampu nne zenye uwezo wa kusukuma lita millioni 4 kwa siku, kulaza bomba la chuma la kusukumia maji lenye kipenyo cha 400mm takribani 17km kutoka Kibamba mpaka Kisarawe Minarani, ambapo linajengwa tanki kubwa lenye ujazo wa lita million 6.

Mkuu huyo wa Wilaya ameongeza kuwa hatua zilizopigwa mpaka sasa kwenye mradi huo ni kuagizwa kwa mabomba, kusafisha njia za kulaza mabomba, uchunguzi wa udondo eneo litakalojengwa tanki pamoja na vifaa vitakavyotumika kujenga tanki hilo.

Katika kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa haraka Jokate amesema Mkandarasi anatakiwa kumilisha ujenzi wa mradi huo ifikapo Septemba 17, mwaka 2019.