Tanzania imepata fursa ya kuingia kwenye shindano la hifadhi ya mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ulimwenguni linaloendeshwa na shirika la hifadhi ya mazingira na wanyamapori ulimwenguni- WWF likishirikisha nchi kumi na nane na zaidi ya miji na majiji mia moja.
Afisa anayeshughulikia nishati jadidifu katika shirika la WWF Bi Philipina Shayo amesema lengo la shindano hilo ambalo kwa Afrika ni nchi mbili pekee zinazoshiriki ambazo ni Tanzania na Afrika Kusini ni kuona ni jinsi gani nchi hizo zitakavyotumia rasilimali zilizonazo kukabliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Majiji ya Arusha na Dar es salaam na manispaa ya moshi ndiyo yaliyoteuliwa kuwakilisha nchi katika shindano hilo.
Meya wa mji wa Moshi Japhary Michael anasema nguvu kubwa itaelekezwa kwenye upatikanaji wa nishati mbadala huku jiji la Arusha likiweka mikakati ya kuendelea kuliweka jiji safi kwa kuboresha Dampo lake la kisasa.
Awali akizindua rasmi mradi wa maandalizi ya shindano hilo uliopewa jina la Earth Hour City Challenge Meya wa Jiji la Arusha Gaudence Lyimo anasema mafanikio yatafikiwa kwa kuwashirikisha wadau wote.