Wakulima wadogo wakiwa shambani wakilima kwa Jembo la kuvutwa kwa Ngombe.
Kauli hiyo imetolewa na mtafiti wa masuala ya pembejeo za kilimo toka Chuo Kikuu cha Dar es salaam bw. Balton Kanje katika semina iliyowakutanisha wadau na wataalamu wa kilimo toka wilaya ya Njombe na Wanging'ombe wakati wa kujadili matokeo ya andiko la pembejeo feki.
Amesema utafiti huo uliofanywa na UDBS-CPRA, kwa ufadhili wa best dialogue kupitia Baraza la Kilimo Tanzania [Agricultral Council of Tanzania[ACT] imebaini kuwepo kwa ongezeko la pembejeo feki ambazo zimekuwa zikileta athari kwa wakulima na jamii nzima kwa ujumla.
Aidha amesema kupitia utafiti huo umebaini kuwa asilimia 5 hadi 7 kati ya pembejeo zinazoingizwa nchini ni feki huku sababu kubwa zikitajwa kuwa ni pamoja na uwezo mdogo wa wauzaji na watumiaji katika kutambua kama pembejeo hizo si halisi.
Amesema sababu nyingine ni tamaa na ukosefu wa uadilifu miongoni mwa wafanyabiashara wa pembejeo hizo, udhaifu wa utekelezaji wa sheria na kanuni pamoja na uhaba wa wataalamu wa kilimo na uwezo mdogo wa wakulima katika kununua pembejeo halisi.
Aidha mtafiti huyo ameongeza kuwa kati ya madhara yanayotokana na pembejeo hizo feki ni pamoja na uzalishaji mdogo wa mazao pamoja na hasara kutoka kwa wakulima ambao wananunua pembejeo hizo bila kujua ubora wake.
Baadhi ya wadau wa Kilimo walioshiriki semina hiyo wametumia fursa hiyo kuitaka serikali pamoja na jamii nzima kushirikiana katika kudhibiti pembejeo feki zikiwemo za mahindi na nafaka nyingine pamoja na kufanya utafiti wa udongo katika maeneo mbalimbali mkoani Njombe kabla ya kuleta mbegu hizo.