Friday , 16th Jan , 2015

Mkuu wa idara ya habari na mawasiliano wa mfuko wa maendeleo ya jamii Tanzania Tasaf, bi. Zuhura Mdungi, amesema Tanzania imekuwa ni nchi ya mfano wa kuigwa kwa nchi za Afrika, kuwa na mafanikio makubwa ya muda mfupi ya utekelezaji wa TASAF.

Mkuu wa idara ya habari na mawasiliano wa mfuko wa maendeleo ya jamii Tanzania Tasaf, bi. Zuhura Mdungi

Akizungumza wilayani Mbarali mkoani Mbeya, Bi Mdungi amesema katika halmashauri za wilaya nane nchini zilizoanza na mpango wa uhamilishaji fedha, zimeonesha matokeo makubwa na maisha ya wananchi waliofikiwa kwenye kaya masikini yameimarika.

Amesema TASAF awamu ya tatu, imepangwa kutekelezwa kwa kipindi cha miaka kumi katika awamu mbili, ingawa mpango huu unahitaji uwekezaji mkubwa, unalenga kusaidia kaya zinazoishi katika hali duni zaidi ya umaskini.

Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya, ilikuwa moja ya wilaya za majaribio, wamefikiwa zaidi ya walengwa 2,000, wananchi kutoka kwenye kaya zilizonufaika na ruzuku ya msingi wamepata unafuu wa maisha hususan watoto na akina mama wajawazito kupata lishe bora, huduma za afya na Elimu.

Awamu ya tatu ya TASAF ilizinduliwa na Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Agosti, 15 / 2012 Dodoma, na awamu hii ya mpango huu inachangia kufikiwa kwa malengo ya mpango wa kukuza uchumi na kupunguza umasikini MKUKUTA..