Akizungumza katika siku ya kwanza ya mkutano wa wakuu wa nchi zinazounda Ukanda wa Kati wa Maendeleo, Rais Kikwete amesema mipango hiyo iangalie pia namna ya kuboresha mawasiliano na upatikanaji wa nishati ya uhakika, ambapo ameshauri umuhimu wa ushirikiano ambapo nchi yenye hazina kubwa ya nishati inaweza kusambaza na kuuza kwa nchi jirani, na vivyo hivyo kwa suala la mawasiliano.
Aidha, Rais Kikwete amesema Tanzania inakusudia kupunguza vizuizi vya barabarani katika barabara kuu kati ya Dar es Salaam na nchi jirani za Uganda, Rwanda na Burundi, kutoka vizuizi zaidi ya kumi vilivyopo sasa hadi vizuizi vitatu.
Kwa upande wake, Rais wa Uganda Yoweri Museveni amewataka wananchi wa nchi zinazounda ukanda wa kati wa maendeleo kufanya kazi kwa bidii huku wakitambua vikwazo vinavyozuia ustawi wa jamii ambavyo ni rushwa, ukosefu wa usalama, ukosefu wa masoko na ukosefu wa miundombinu bora.
Mkutano huo wa siku mbili, unakutanisha wakuu wa nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ukiwa na lengo la kuchochea maendeleo katika ukanda wa kati kupitia uboreshaji wa miundombinu ya usafirishaji mizigo na bidhaa, mkutano ambao pia umewakutanisha wadau wa sekta ya usafiri, taasisi za kikanda pamoja na vyombo vya kifedha ambavyo ni wafadhili wakuu wa miradi ya miundombinu.
Marais Paul Kagame wa Rwanda, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya na Rais Laurent Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambao walitarajiwa kuhudhuria mkutano huo wameshindwa kuhudhuria na badala yake wametuma waakilishi wao.
Wakati huo huo Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki nchini Tanzania Dkt. Harrison Mwakyembe ametaka kuwepo kwa ushirikiano zaidi kati ya mahakama kuu ya Tanzania na Mahakama ya Afrika Mashariki kwa lengo la kurahisisha utendaji wao wa kazi.
Akizungumza leo Jijini Dar es Salaam katika mkutano wa pamoja kati ya majaji wa mahakama kuu ya Tanzania na watendaji wakuu wa mahakama ya Afrika Mashariki Dkt. Mwakyembe amesema mahakama hizo mbili zikiongeza kasi ya ushirikiano zitaweza kuleta ufanisi wa kiutendaji katika mahakama za Tanzania.
Amesema kwa kutumia mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki mahakama hizo zitaweza kupokea kesi na kuzishughulikia kwa ukaraibu zaidi na hivyo kuondoa lawama kwa wananchi juu ya kuchelewa usikilizwaji wa kesi.