Monday , 28th Jul , 2014

Takwimu zinaonesha kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la maambukizi ya virusi vya homa ya ini kwa vijana wanaotumia dawa za kulevya Jijini Dar es Salaam, nchini Tanzania.

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt Seif Rashid.

Akiongea na EATV jijini Dar es Salaam leo, katika siku ya Maadhimisho ya Homa ya Ini duniani, Meneja mafunzo wa kituo cha madaktari wa ulimwengu wanaowahudumia watumiaji wa dawa hizo jijini Dar es Salaam, Damal Lukas amesema katika wilaya ya Temeke kuna zaidi ya asilimia 18 na Kinondoni ni zaidi ya asilimia 70 ya vijana waliopimwa homa ya Ini na kubainika kuwa na virusi vya homa hiyo.

Kwa upande wao vijana waliokuwa wakitumia dawa za kulevya kwa muda mrefu na baadaye kuacha, wamesema homa ya Ini imewaathiri baadhi yao kwa kiasi kikubwa kutokana na kuambukizana kupitia damu pamoja na kufanya mapenzi pasipo kutumia kinga hali inayotokana na mwamko duni wa kujali afya zao.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani takribani watu milioni 150 wanaishi na virus vya homa ya Ini, huku watu milioni 3 mpaka 4 huambukizwa virusi hivyo kila mwaka na watu laki 3 mpaka Nne hufa kila mwaka kwa homa ya Ini Duniani.

Wakati huo huo, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii nchini Tanzania imeahidi kuamsha ari ya wanafunzi kupenda masomo ya Sayansi ili kuongeza idadi ya wataalam wa fani za sayansi hususani wale wa somo la Kemia.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Dk. Charles Pallangyo, ametoa ahadi hiyo leo jijini Dar es Salaam, ambapo amesema Tanzania inakabiliwa na uhitaji mkubwa wa wataalamu wa fani ya kemia wanaohitajika katika fani mbalimbali za utabibu wa afya na magonjwa ya binadamu.

Ametaja baadhi ya mbinu zitakazotumiwa na wizara hiyo ni pamoja na kuendeleza utaratibu uliopo sasa wa kutoa motisha kwa wanafunzi wa kidato cha Nne na cha Sita wanaofanya vizuri katika masomo ya Sayansi, hususani yale yenye uhusiano moja kwa moja na taaluma ya utabibu wa afya ya binadamu.