Monday , 22nd Dec , 2014

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa kamwe Tanzania, kama ilivyo nchi nyingine yoyote duniani, haiwezi kuendelea kwa kutegemea ramli bila kuwekeza kwenye maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete

Aidha, Rais Kikwete ametaka watanzania kuacha mwenendo wa kutumia ubishi wa kisiasa kutafuta majawabu ya changamoto za maendeleo akisisitiza kuwa majawabu ya maendeleo yatapatikana katika maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Aidha, Rais Kikwete amewataka Watanzania kuongeza kasi yao ya matumizi ya internet akisema kuwa mfumo huo wa habari na mawasiliano ni chimbuko kubwa la elimu ikiwemo elimu ya sayansi kuliko kutegemea kupata elimu hiyo katika magazeti.

Rais Kikwete aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati alipozungumza katika Mahafali ya Pili ya Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela iliyoko Tengeru, Arusha, taasisi ambayo hutoa shahada za juu za uzamili na uzamivu katika sayansi, teknolojia na tafiti za kisayansi.

Akizungumza baada ya yeye mwenyewe kuwa ametunukiwa Digrii ya Heshima ya Uzamivu (PhD Honoris Causa) katika mahafali hayo ya pili, Rais Kikwete alielekeza sehemu kubwa ya hotuba yake kuelezea umuhimu wa maendeleo ya sayansi na teknolojia katika uhai na maendeleo ya Tanzania na taifa lolote duniani.

“Somo tunalolipata ni kwamba hakuna mazingaombwe wala njia ya mkato ya kujipatia maendeleo ya juu. Hatuna budi kuwekeza katika kuendeleza sayansi na teknolojia nchini, kama kweli tunataka kutoka hapa tulipo. Hakuna ramli wala pumba za uchawi zinazoweza kuendeleza nchi yetu hata ukiimwaga pumba hiyo katika kila njia panda ya barabara na sehemu zote za Tanzania. Bado Tanzania haitabadilika hata inchi moja,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:

“Hatuna budi kuwekeza zaidi katika kufundisha wanasayansi, na katika tafiti na ujenzi wa miundombinu ya kuwawezesha wanasayansi kufanya tafiti zao. Kwa muda mrefu sana hili ni eneo ambalo hatukulipa uzito unaostahili.”

Alisisitiza: “Tumefundisha na kuwekeza sana katika kuwaandaa vijana wetu katika fani za sayansi ya jamii, uongozi, siasa, sheria na biashara. Pamoja kada hizo kuwa muhimu, lakini wanasayansi ni muhimu zaidi.”

Rais Kikwete amesema kuwa watanzania hawana budi kusaka elimu yenye manufaa zaidi ya maendeleo siyo kushinda katika mambo ambayo hayana manufaa kama vile kushinda kwenye ubishi wa kisiasa. “Watanzania kwenye ubishi wa siasa usiseme – kila mtu fundi. Wanatumia siasa kujadili maendeleo na kazi ni kulaumu watu wengine tu.”

Kuhusu umuhimu wa kusaka elimu, Rais amesema kuwa Watanzania wanapaswa kusaka elimu kila inapopatikana. Kwenye internet, kwa mfano, ni mahali ambako unapata kila kitu duniani. Elimu yetu hii ya kutafutwa kwenye magazeti haitupeleki mbali – magazeti yenyewe yamejaa siasa tupu, nani kashinda kura zaidi kuliko mwingine nani kashinda kidogo