Thursday , 21st Jan , 2016

Shirika la ugavi wa Umeme (TANESCO),mkoani Rukwa, limewatahadharisha wateja wake mkoani humo, kuwa zoezi la kuwasaka wateja wasiokuwa waaminifu na wanaoiba umeme bila ya kuulipia ni la kudumu.

Mmoja wa Mafundi wa Umeme akiwa anaangalia mita ya Mteja kama imechezewa au la!!

Meneja wa shirika hilo mkoani Rukwa Mhandisi Herini Mhina, amesema hadi sasa tayari wamewakamata wateja zaidi ya 15 kwenye manispaa ya sumbawanga, wanaochezea mita ili waweze kutumia umeme bila ya kuulipia na hatua mbalimbali kuchukuliwa dhidi yao.

Aidha Mhandisi Mhina ameongeza kuwa zoezi hilo linaenda sambamba na ufuatiliaji wa madeni kwa wateja mbalimbali yanayofikia kuwa zaidi ya shilingi milioni 50 mkoani humo.

Kwa upande wao baadhi ya wakazi wa manispaa ya Sumbawanga wakiwemo na watuhumiwa wa matumizi ya umeme bila ya malipo, wameunga mkono zoezi hilo ambalo linalenga kulinusuru shirika hilo la ugavi wa umeme, linalopoteza mamilioni ya fedha kwa kutoa umeme usiolipiwa na wateja wasiokuwa waaminifu,wengi wao wakiwa ni wateja wakubwa.