Friday , 7th Aug , 2015

Shirika la Hifadhi za Taifa TANAPA limezindua kampeni maalum ya miezi sita yenye lengo la kuwahamasiha watanzania kujenga utamaduni wa kutembelea hifadhi za taifa kila mara ili kuongeza utalii wa ndani.

Tembo ni moja kati ya Wanyama wanaotumika sana kutazamwa katika utalii nchini Tanzania

Hali hiyo inatokana na kasumba iliyojengeka miongoni mwa watanzania kuwa utalii hufanywa na wageni kutoka nje ya nchi pekee.

Tanzania ni moja kati ya mataifa yenye vivutio vingi vya utalii duniani ikiwa na hifadhi za taifa 16.

Kwa miaka mingi imekuwa ikipokea wageni kutoka mataifa mbalimbali ambao huja kutembelea ili kujionea wanyama, ndege na mimea asilia.

Waziri wa Maliasili na Utalii Lazaro Nyalandu ndiye aliezindua kampeni hii Julai Mosi na itafikia kikomo Desemba 31 mwaka huu.

Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini imezungukwa na baadhi ya hifadhi za taifa. Hifadhi hizo ni pamoja na Katavi, Ruaha na Kitulo.

Aidha wamesema kuwa ili kuongeza hamasa TANAPA imeandaa zawadi kwa watanzania wakaotembelea hifadhi hizo Zaidi ya mara tatu ikiwemo kulala kwenye hoteli zenye hadhi ya Nyota tano.

Wanafunzi wa shule za sekondari wao wanaona kuna haja ya kuanzisha mitaala maalum kwenye shule na vyuo huku wakitaka mamlaka husika kuongeza kasi ya kutangaza vivutio hivyo.