Picha hii inaeleza moja ya matukio ya unyanyasaji wa kijinsia yanayoendelea sehemu mbali mbali nchini Tanzania.
Hayo yamebainishwa ndani ya utafiti uliofanywa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake nchini Tanzania TAMWA katika wilaya kumi nchini, utafiti uliokuwa unaangalia ukubwa na chanzo cha tatizo la ukatili wa kijinsia.
Utafiti huo umefanywa kupitia awamu ya pili ya mradi wa elimu kuhusu haki za kijinsia na uwezeshaji wanawake kiuchumi ujulikanao kama GEWE II, ambao unatekelezwa kwa pamoja na taasisi za TAMWA, Chama Cha Wanasheria Wanawake nchini Tanzania TAWLA, Chama cha Wanasheria Wanawake Zanzibar - ZAFELA na kituo cha Usuluhishi wa masuala ya kijamii na kijinsia - CRC.
Akitoa matokeo ya utafiti huo jijini Dar es Salaam leo, Kaimu Mkurugenzi wa TAMWA Bi. Gladness Munuo amesema kitendo hicho ni hatari kwa afya ya wasichana husika kwani wanaweza kupata madhara makubwa ya kiafya na kisaikolojia ikiwemo kutoweza kupata watoto katika maisha yao.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TAMWA Bi. Rose Reuben amesema kuwa utafiti huo umeonyesha kupungua kwa kiwango cha ukatili wa kijinsia, licha ya kuwepo kwa maeneo machache ambako bado vitendo hivyo vimekuwa vikiendelea.
Ametaja sababu zilizochangia kupungua kwa matukio ya unyanyasaji wa kijinsia kuwa ni elimu ambayo imekuwa ikitolewa kwa wananchi kuhusu madhara na ubaya wa ukatili wa kijinsia.