Baraza la Mazingira nchini Tanzania (NEMC) limewataka wananchi waliopo kwenye maeneo hatarishi na yaliyopo katika mikondo ya maji likiwemo la mto Msimbazi jijini Dar es Salaam kuhama na kuacha maeneo hayo wazi kwa ajili ya kupitisha maji ili kuepusha kutokea mafuriko na magonjwa kama kipindupindu.
Akiongea leo jijini Dar es Salaam wakati wa zoezi la bomoa bomoa linaloendelea katika eneo la Kinondoni Mkwajuni kwa wakazi waliojenga kwenye mkondo wa bonde la mto Msimbazi Mwanasheria Mkuu wa NEMC Bw. Machali Heche amesema hilo ni zoezi litakaloendelea nchi nzima.
Bw. Heche amewataka waliojenga ndani ya umbali wa mita sitini kuondoka wenyewe kwenye maeneo oevu ikiwa ni pamoja na maeneo ya karibu na mito na bahari na kuwa zoezi hilo bado linaendelea katika maeneo yote ambayo yalishatolewa taarifa kwa wakazi wahusika.