Chama cha Wafanyakazi Madereva nchini Tanzania (TADWU) kimetangaza rasmi kusitisha huduma za usafiri kwa madereva kuanzia wiki ijayo kwa kipindi cha siku tano ama zaidi kwa madai kwamba madereva watakuwa wote katika mafunzo yanayolenga kuwafundisha namna ya kuzuia ajali zinazotokana na uzembe wakati wakiwa barabarani.
Naibu Katibu Mkuu wa (TADWU), Bw. Rashid Saleh amesema madereva wote wakiwemo wa mabasi ya abiria watalazimika kusitisha huduma kwa kuwa watakuwa wakishiriki mafunzo hayo ambayo yanatokana na elimu waliyopewa viongozi wa chama hicho wakati wa mkutano kati yao na Wizara ya Kazi na Ajira
"Semina yetu inamuhusu dereva na itasaidia katika kuondoa ajali kutokana na semina hiyo huduma ya mabasi itasitishwa kutokana na semina hiyo kuhusisha madereva na baada ya hapo watarudi kazini" alisema Saleh.
Akizungumzia hatua hiyo ya chama cha wafanyakazi madereva (TADWU), Katibu Mkuu wa chama cha wamiliki wa mabasi nchini (TABOA) Bw. Ernea Mrutu amesema mafunzo hayo hayapo kisheria kwa kuwa waajiri hawana taarifa nayo na hivyo dereva yoyote atakayejaribu kushiriki atakuwa amejifuzisha kazi.
Mrutu amesema wote watakaoshiriki mafunzo hayo watakuwa wamejifukuza kazi kisheria kutokana na kuwa mabasi yatafanya kazi kama kawaida na kuwataka abiria wafike kwenye vituo kama kawaida.