Saturday , 18th Jun , 2016

Mwenyekiti Mtendaji wa Sekta Binafsi Nchini (TPSF), Godfrey Simbeye, amewataka vijana kujituma kwa hali na mali katika kutumia fursa zilizopo nchini ili ziweze kuwazalishia kipato ikiwa ni pamoja na kujiajiri na kuajiri vijana wengine.

Bwn. Simbeye ameyasema hayo aliposhiriki kama mgeni rasmi katika hafla ya kutoa tuzo za kuwapongeza wajasiriamali wadogo wanaofanya shughuli mbalimbali nchini zilizoandaliwa na Tanzania Young Prossional Awards (TAYPA) mwaka 2016 zilizofanyika Jijini Dar es salaam.

‘’Uchumi wetu ni mdogo ila watu ni wengi hii inaashiria kwamba bado hatujaweza kutumia rasilimali zilizopo nchini vizuri katika kuleta maendeleo’’- Amesema Simbeye.

Aidha amewashukuru TAYPA kwa kufanya tukio la kutoa zawadi kwa vijana ambao wanafanya hizuri katika sekta mbalimbali kwa kujiajiri na kutengeneza miradi inayoonyesha utayari wao katika kulitumikia taifa.

Vijana mbalimbali kutoka maeneo tofauti ya nchi wameweza kupata tuzo za TAYPA kwa mchango wao na juhudi wanazozionyesha katika sekta mbalimbali za elimu, kilimo, utalii na utafiti ambao baada ya kuuingiza katika matendo umeweza kusaidia watu wengine.