Friday , 4th Jul , 2014

Kuwepo kwa malumbano ya kimaslahi baina ya Chama Tawala na kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi UKAWA, kumetajwa kuwa ni kikwazo kitakachosababisha kutokuwepo kwa muafaka wa kupata Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mwanasheria mkuu mstaafu wa serikali Jaji mstaafu Mark Bomani (wa kwanza kulia) akiwa katika mkutano wake na waandishi wa habari hivi karibuni.

Hayo yamesemwa Jijini Dar-es-Salaam na Mwanasheria Mkuu wa zamani Jaji mstaafu Mark Bomani ambapo ameeleza si vyema kuendelea kuwepo kwa mifarakano baina ya pande zote mbili ili Katiba iweze kupatikana.

Hata hivyo Jaji Bomani amependekeza Bunge maalumu la katiba kuweka kando kwanza suala la idadi ya serikali na kujadili mambo mengine ambapo amewasihi UKAWA kurudi bungeni.

Kauli ya Jaji mstaafu Bomani imekuja siku chache baada ya waziri mkuu Mizengo Pinda kutoa wito kwa UKAWA kurejea bungeni na kwamba tofauti zilizopo katika mchakato huo zinaweza kumalizwa kwa mazungumzo.

Hata hivyo viongozi wa UKAWA kwa upande wao wamesisitiza kuwa kamwe hawatorudi na kuhudhuria vikao vya bunge maalumu la katiba kutokana na kile walichodai kuwa mchakato huo umehodhiwa na chama tawala CCM.